Matokeo ya kidato cha nne:kufeli kwaongezeka, wasichana wangara

Kufeli kwaongezeka na wasichana wang’ara kidato cha nne
Thursday, 27 January 2011 08:40
0diggsdigg

Fidelis Butahe na Hussein Issa
BARAZA la Mitihani la Taifa (Necta) limetangaza matokeo ya mtihani wa kidato cha nne uliofanyika Oktoba, 2010 yanayoonyesha kuwa wasichana wanaongoza kwa kiwango cha ufaulu.

Hata hivyo matokeo hayo yameonyesha kuwa kiwango cha ufaulu katika mtihani huo kimeshuka kwa asilimia 22 ilinganishwa na matokeo ya mwaka 2009. Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Joyce Ndalichako, aliwaambia waandishi wa habari wakati akitangaza matokeo hayo jana, kuwa wasichana wamefanya vizuri zaidi kuliko wavulana.

“Kati ya watahiniwa kumi bora, sita ni wasichana na wanne ni wavulana,” alisema Dk Ndalichako na kumtaja kinara wa matokeo hayo kuwa ni Lucylight Mallya kutoka Shule ya Sekondari ya Wasichana ya St Marian iliyopo mkoani Pwani. Hii ni mara ya pili kwa shule hiyo kutoa mwanafunzi bora katika mtihani wa kidato cha nne baada ya Immaculate Mosha aliyeibuka kinara katika matokeo ya mwaka 2009. Kwa mujibu wa matokeo ya mtihani wa mwaka jana, kati ya shule kumi bora katika kundi la shule zenye watahiniwa chini ya 40, saba ni shule za seminari na huku Shule ya Seminari ya Uru inaongoza shule kumi bora katika kundi la shule zenye watahiniwa zaidi ya 40.

Matokeo hayo yanaonyesha kuwa shule kumi za mwisho ni mchanganyiko wa shule za serikali na watu binafsi. Dk Ndalichako alitaja shule kumi bora zenye watahiniwa zaidi ya 40 na mikoa zinakopatikana kwenye mabano kuwa ni Uru Seminari (Kilimanjaro), Marian Girls (Pwani), St Francis Girls (Mbeya), Canossa (Dar es Salaam), Msolwa (Morogoro), Feza Boys (Dar es Salaam), St Mary Goreti (Kilimanjaro), Abbey (Mtwara), St Joseph Semiterambogo (Kigoma) na Barbro-Johansson (Dar es Salaam).

Alieleza kuwa shule kumi bora zenye watahiniwa chini ya 40 ni seminari ya Don Bosco (Iringa), Feza Girls (Dar es Salaam), Maua Seminari (Kilimanjaro), Queens of Apostles Ushirombo (Shinyanga), Sengerema Seminari (Mwanza), Sanu Seminari (Manyara), Bethelsabs Girls (Iringa), St Joseph-Kilocha Seminary (Iringa), Dungunyi Seminary (Singida) na Mafinga Seminary (Iringa). Kwa mujibu wa Dk Ndalichako, shule kumi za mwisho zenye watahiniwa chini ya 40 ni, Sanje (Morogoro), Daluni (Tanga), Kinangali (Singida), Mtanga na Pande (Lindi), Imalampaka (Tabora), Chongoleani (Tanga), Mwamanenge (Shinyanga), Mipingo (Lindi) na Kaoze (Rukwa). Alitaja shule zingine kumi za mwisho katika kundi la shule zenye watahiniwa zaidi ya 40 kuwa ni Changaa (Dodoma), Pande Darajani (Tanga), Igawa (Morogoro), Makata (Lindi), Kolo, Kikore na Hurui (Dodoma), Mbuyuni (Mtwara), Thawi (Dodoma) na Naputa (Mtwara). Dk Ndalichako pia aliwataja watahiniwa kumi bora kitaifa na shule zao kwenye mabano kuwa ni Lucylight Mallya (St Marian), Maria-Dorin Shayo (St Marian), Sherryen Mutoka (Barbro-Johansson), Diana Matabwa (St Francis Girls) na Neema Kafwimi (St Francis Girls). Wengine ni, Beatrice Issara (St Mary Goreti), Johnston Dedani (Ilboru), Samwel Emmanuel (Moshi Technical), Bertha Sanga (Marian Girls) na Bernadetha Kalluvya (St Francis Girls).

Dk Ndalichako alisema kuna wanafunzi 42 kutoka baadhi ya shule walifanya mtihani wakati walikwisha ondolewa katika usajili baada ya kubainika kuwa sifa za kidato cha pili walizowasilisha hazikuwa sahihi. Alizitaja shule hizo na idadi ya wanafunzi kwenye mabano kuwa ni Ujenzi (4), Kahama Muslim (1) St John Seminari (1), Eckernforde (1), Seuta (1), Jamhuri (1) Mdanya New Vision (12) na Mseru (21). Dk Ndalichako alifahamisha kuwa watahiniwa 56 wa kujitegemea waliondolewa kwenye usajili kwa kutokuwa na sifa lakini walifanya mtihani huo. Alivitaja vituo walivyofanyia mtihani watahiniwa hao na idadi yao katika mabano kuwa ni Mwigo (29) na Twitange (27). Dk Ndalichako alisema mtihani huo ulifanywa na watahiniwa 177,021 na asilimia 50.40 ya watahiniwa wote, wamefaulu. Wasichana waliofaulu ni 69,996 sawa na asilimia 43.47 na wavulana ni 107,025 sawa na asilimia 56.28. “Mwaka 2009 watahiniwa waliofaulu walikuwa sawa na asilimia 72.51 ya watahiniwa waliofanya mtihani huo,” alisema Ndalichako

Alisema ubora wa ufaulu kwa kuangalia madaraja waliyopata watahiniwa wa shule unaonyesha kuwa jumla ya watahiniwa 40,388 sawa na asilimia 11.50, wamefaulu katika madaraja I hadi III. “Wasichana waliofaulu katika madaraja I hadi III ni 12,583 sawa na asilimia 7.81 na wavulana ni 27,805 sawa na asilimia 14.62,”alisema Dk Ndalichako. Alisema idadi ya watahiniwa wa kujitegemea waliofaulu mtihani huo ni 46, 064 sawa na asilimia 52.09 ya waliofanya mtihani.

Alisema katika kundi hilo, wasichana waliofaulu ni 22,405 sawa na asilimia 48.41 na wavulana ni 23,659 sawa na asilimia 56.13. Mwaka 2009 watahiniwa wa kujitegemea 49,477 sawa na asilimia 54.12 walifaulu, alisema. Aliongeza kuwa watahiniwa 458,114 wakiwamo wasichana 216,084 sawa na asilimia 47.17 na wavulana 242,030 sawa na asilimia 52.83 ndio waliojisajili kufanya mtihani huo mwaka jana. “Mwaka 2009 watahiniwa waliosajiliwa walikuwa 351,152, hivyo idadi ya watahiniwa imeongezeka kwa watahiniwa 106,962 sawa na asilimia 30.5,” alisema Dk Ndalichako na kuongeza:

“Waliofanya mtihani wa kidato cha nne mwaka 2010 ni 441,426 sawa na asilimia 96.36 na watahiniwa 16,688 ambao ni sawa na asilimia 3.64 ya watahiniwa wote waliosajiliwa, hawakufanya mtihani. “Kuna ongezeko la watahiniwa wa shule 109,329 ambao ni sawa na asilimia 43.0 ikilinganishwa na idadi ya waliosajiliwa mwaka 2009. Watahiniwa waliofanya mtihani walikuwa 352,840 sawa na asilimia 97.04, watahiniwa 10,749 sawa na asilimia 2.96 hawakufanya mtihani,” alisema Dk Ndalichako.

Alifahamisha kuwa mwaka 2009 watahiniwa wa kujitegemea waliosajiliwa walikuwa 96,892 na 2010 kulikuwa na watahiniwa 94,525 ikimaanisha kulikuwa na upungufu wa watahiniwa 2,367 sawa na asilimia 2.44 ikilinganishwa mwaka 2009. “Watahiniwa 88,586 wakiwemo wasichana 46,358 na wavulana 42,228 walifanya mtihani huo, watahiniwa wa kujitegemea 5,939 sawa na asilimia 6.28 hawakufanya mtihani.

Shule zenye watahiniwa zaidi ya 40 zilikuwa 3,194 na zenye watahiniwa chini ya 40 zilikuwa 489. Akizungumzia matokeo ya mtihani wa maarifa (QT), alisema watahiniwa waliosajiliwa walikuwa 26,540 kati yao wasichana ni 16,101 na wavulana 10,439. Alisema mwaka 2009 jumla ya watahiniwa 25,040 walisajiliwa kufanya mtihani huo kukiwa na ongezeko la watahiniwa 1,500, sawa na asilimia 5.99 ikilinganishwa na mwaka 2009 na kwamba jumla ya watahiniwa 23,585, sawa na asilimia 88.87 ya waliosajiliwa walifanya mtihani huo. Alisema katika mtihani wa maarifa (QT) jumla ya watahiniwa 8,295 sawa na asilimia 35.17 ya waliofanya mtihani huo wamefaulu ikilinganishwa na asilimia 28.82 ya waliofaulu mwaka 2009. Alisema kuwa kiwango cha ufaulu kwa mtihani wa maarifa kimeongezeka kwa asilimia 6.35 ikilinganishwa na wamaka 2009.

“Jumla ya watahiniwa 311 wa mtihani wa kidato cha nne na watahiniwa 2 wa mtihani wa maarifa (QT) wamefutiwa matokeo yao yote ya mtihani kwa mujibu wa kifungu cha 52 (b) cha kanuni za mtihani baada ya kubainika kuwa walifanya udanganyifu katika mtihani huo,” alisema Dk Ndalichako. mwisho

Published in: on January 28, 2011 at 2:53 pm  Comments (1)  
Tags:

The URI to TrackBack this entry is: https://marafikiwavitabu.wordpress.com/2011/01/28/matokeo-ya-kidato-cha-nnekufeli-kwaongezeka-wasichana-wangara/trackback/

RSS feed for comments on this post.

One CommentLeave a comment

  1. Lakini hatujui hatma ya waliofeli


Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s

%d bloggers like this: